TUKATAE SILAHA ZA NYUKLIA

Silaha za nyuklia ni tisho kubwa kwa uhai wa binadamu na dunia yote kwa jumla. Kumaliza silaha hizo ni kazi inayoendelea kuwa ya dharura.

Pakua kijitabu
TUKATAE SILAHA ZA NYUKLIA

Mataifa mengi ya ulimwengu yamejitolea kwa dhati kwa lengo hili, kwa kuitikia na kutia sahihi Mkataba wa Kupiga Marufuku Silaha za Nyuklia ambao ulianza kutekelezwa 2021.

Hata hivyo, mataifa tisa bado yanamiliki silaha hizo hatari zinazoweza kusababisha uharibifu mkubwa na maangamizi, na hivyo kukaidi kanuni mpya za kimataifa na mapenzi ya raia wao. Kila mwaka, nchi hizo zinafuja mabilioni ya dola kwa kuimarisha na kupanua viwanda na hifadhi zao za zana hizo za vita.

Mashindano makali ya uundaji wa zana za nyuklia yanaendelea. Tisho la kutumiwa kwa silaha za nyuklia, iwe ni makusudi au kimakosa na kwa bahati mbaya, lingali kubwa sasa kama ambavyo limekuwa hapo awali. Nyakati zote tupo katika hali ambapo uamuzi wowote mbaya unaweza kusababisha maangamizi ulimwenguni.

Ili kuzuia uharibifu usio na kifani ambao silaha za nyuklia zinakusudiwa kusababisha, serikali hazina budi kuchukua hatua za dharura kuangamiza zana hizo kama hakikisho la pekee la kukomesha kuendelea kuzitumia na kuzifanyia majaribio.

Lakini hilo litafanyika kwa sharti kwamba watu wote kila mahali wataamka na kusisitiza hatua zifaazo zichukuliwe.

Silaha hatari zaidi ulimwenguni

Silaha za nyuklia ndizo haribifu zaidi, zisizobagua na za kinyama zilizowahi kuundwa. Bomu moja lina nguvu tosha za kuharibu jiji nzima na kusababisha maafa ya makumi ya maelfu, iwapo sio mamilioni ya watu.

Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limezitaja silaha za nyuklia kuwa na “nguvu haribifu za kipekee kwa mateso yasiyo na kifani zinazosababisha … na ni tisho kwa mazingira, vizazi vijavyo na hasa maisha ya binadamu”.

Silaha hizo hutoa kiasi kikubwa cha mnururisho, huchafua hewa, ardhi, maji na miili yetu na kusababisha madhara yanayoenea kutoka taifa moja hadi jingine na vizazi hadi vingine.

Ilimradi silaha hizo zipo, pana hatari kubwa kuwa zitatumika tena, na matokeo yake yatakuwa maangamizi, ikiwa ni pamoja na kwa watu wa mataifa yasiyohusika na mapigano ambapo zinatumika.

Barakoa za kujikinga na gesi hazitoi kinga yoyote dhidi ya miale nururishi ya gamma. Picha na: Ricky Pitman

Athari za silaha za nyuklia

Joto

Silaha ya nyuklia ikilipuliwa, hutoa joto kali. Karibu kila kitu na kila mtu katika kitovu cha mlipuko hugeuka mara moja kuwa jivu na mvuke.

Wimbi kubwa la moto ambao kipimo cha halijoto ya kitovu chake huwa ni zaidi ya digrii milioni moja kwa vipimo vya Celsius, hupaa juu angani na halijoto chini ardhini hufika digrii maelfu kadhaa na huwa juu zaidi kuliko ya jua.

Joto hilo kali huwasha moto unaoenea mbali, unarusha moshi wenye sumu hewani pamoja na gesi zinazoweza kuunguza. Moshi na gesi hizo zikiungana husababisha dhoruba au mvua kubwa ya moto.

Hata watu walio umbali wa makumi ya kilomita kutoka eneo la mlipuko wa bomu la nyuklia hupata majeraha kali na hatari ya kuchomeka yawezayo kuua, ilhali walio mbali zaidi hupoteza uwezo wa kuona kutokana na nuru kali ya silaha hizo.

Mlipuko

Silaha ya nyuklia hutoa pia ukuta mkubwa unaoenda kasi wa mvuke wenye nguvu nyingi ujulikanao kama wimbi la kishindo linalosafiri mbali kwa kilomita nyingi.

Wimbi hilo hurusha watu hewani, linawakosesha fahamu, linapasuapasua miili yao na kuharibu mapafu kabisa.

Majengo katika maeneo makubwa hubomolewa na watu wengi hupondwa na kuachwa maiti. Vitu vingine vilivyofunguka hupeperushwa angani kama makombora.

Hata magorofa makubwa yaliyokorogewa na mengine ya chuma huharibiwa na nguvu za mlipuko.

Mnururisho

Mfululizo wa madhara yanayosababisha mlipuko hutoa kiasi kikubwa cha mnururisho unaobadilika kuwa ioni, unapenya ndani ya miili ya watu, unaharibu au unadhuru viini vyao na kusababisha magonjwa.

Hata katika umbali wa kilomita kadhaa kutoka eneo la mlipuko, watu hupata mnururisho mkubwa kiasi cha kusababisha vifo kutokana na sumu yake kali.

Ishara zake ni pamoja na kutapika, ufizi wa meno kuvuja damu, kuharisha na nywele zote kung’oka. Waathiriwa wengi hufa miezi michache baada ya shambulizi.

Baadhi ya wanaopatwa na madhara hayo hupona lakini hufa baada ya miaka kadhaa au hata miongo kutokana na kansa na magonjwa mengine yanayohusishwa na madhara ya muda mrefu ya mnururisho.

Baadhi ya manusura huonyesha kasoro za kromosomu, na madhara mengine ya kinasaba yawezayo kupasishwa vizazi vijavyo.

Cheche za mnururisho zinazotokana na mlipuko wa bomu la nyuklia

Silaha ya nyuklia husababisha pia wingu kubwa lenye umbo la uyoga ambalo hunyonya vumbi na takataka zenye uwezo wa kunururisha, zinakuwa kama mnara wa cheche, na kurushwa hewani.

Mkondo wa upepo hutawanya cheche hizo hewani na hatimaye zinaanguka duniani na kuenea pakubwa.

Cheche hizo za mnunurisho zinazotokana na mlipuko wa silaha ya nyuklia husababisha hatari za afya hapo hapo na pia baada ya muda mrefu hata kwa watu walio mbali na kitovu cha mlipuko. Baadhi ya atomi nururishi huendelea kuwa hatari kwa muda mrefu, zinachafua udongo, maji na bidhaa za chakula.

Sumaku umeme

Silaha ya nyuklia ikilipuliwa katika maeneo ya juu, hutoa mapigo mazito ya sumaku umeme ambayo huharibu vifaa vya kielektroniki katika sehemu kubwa. Mawasiliano ya simu, uwezo wa kutumia intaneti na teknolojia za huduma za benki huvurugwa kabisa.

Madhara hayo yalionekana kwa mara ya kwanza katika enzi ya majaribio ya silaha za nyuklia angani na maeneo yaliyoinuka juu kutoka kwa usawa wa bahari. Marekani ilipofanya jaribio la kulipua silaha ya nyuklia katika anga za juu umbali wa kilomita 400 juu ya kisiwa cha matumbawe cha Johnston katika Bahari ya Pacific, mlipuko uliharibu taa za barabara na simu katika Hawaii, umbali wa zaidi ya kilomita 1,450.

Bomu lenye uwezo wa kusababisha madhara makubwa likilipuliwa katika maeneo yaliyoinuka juu kutoka kwa usawa wa bahari, linaweza kuharibu vifaa vya kielektroniki katika bara lote.

Athari za mlipuko katika jaribio la kulipua silaha za nyuklia kwenye jumba la majaribio lililopo Jimbo la Nevada, Marekani. Picha na: Serikali ya Marekani

Hatari kubwa kwa watoto

Watoto wachanga na wakubwa huwa hatarini kubwa ya kuathiriwa na silaha za nyuklia.

Ni rahisi kwao kufa kutokana na majeraha ya kuchomeka wakilinganishwa na watu wazima (kwani ngozi zao ni nyembamba na nyepesi), majeraha kutokana na milipuko (ikitiliwa maanani udhaifu wa miili yao) na ugonjwa uletwao na mnururisho mkali (kwani wana chembe nyingi za uhai zinazokua na kugawanyika kasi).

Kadhalika, huwa sio rahisi wao kujinusuru kutoka kwa majengo yaliyobomoka na kuchomeka au kuchukua hatua nyingine kufuatia mlipuko kwa lengo la kuongeza nafasi zao za kuponea na kuendelea kuishi.

Mtoto apokea matibabu ya majeraha ya kuchomeka kufuatia kuangushwa kwa bomu la nyuklia katika Nagasaki mnamo 1945. Picha na: Yasuo Tomishige

Majira ya baridi kali ya nyuklia na njaa

Silaha za nyuklia ndizo zana za pekee zilizowahi kuundwa zenye uwezo wa kuharibu aina zote za uhai na hali nyingine za maisha zisizoelezeka kwa urahisi duniani.

Silaha mia moja au zaidi zikitumia kushambulia miji mikubwa, masizi na moshi kutoka kwa mawimbi ya moto zinaweza kuweka pazia la kufunika dunia yote na kuzuia miale ya jua kwa zaidi ya mwongo mmoja, hivyo basi kusababisha kushuka kwa halijoto duniani – athari ijulikanayo kama majira ya baridi kali ya nyuklia.

Ikiwa imetumbukizwa katika giza totoro, dunia inaweza kufikia kiwango cha kuganda, hata katika mazingira ya joto. Mimea ya chakula itaangamizwa na kilimo duniani kuporomoka, na kusababisha njaa kubwa na kuvunjika kwa jamii.

Majanga ya maradhi ya kuambukizana na ugomvi kuhusu rasilmali haba zitaenea. Watu wanaokabiliwa na utapia mlo watakuwa hatarini kubwa ya kufa.

Hata inayojulikana kama vita ndogo ya silaha za nyuklia – ikihusisha sehemu ndogo tu ya silaha za nyuklia duniani – inaweza kusababishia watu duniani hatari ya kufa njaa.

Vita kama hiyo inaweza kudhoofisha ozoni, isababishe ongezeko kubwa la aina fulani za kansa na kuangamiza viumbe na mimea wa baharini na majini. Aina nyingi za mimea na wanyama zitakabiliwa na tisho la kufa na ulimwengu utapatwa na uharibifu usioweza kugeuzika.

Kulazimisha watu kuhama na kuporomoka kwa uchumi

Kwenye vita ya nyuklia, mamilioni ya watu wakifikiwa na cheche za mnururisho zinazotokana na mlipuko wa bomu watalazimika kuhamia nchi jirani wakitafuta makao ya dharura, chakula na maji yasiyo na sumu, pamoja na huduma za matibabu. Idadi ya watu wanaotafuta makao nje ya makwao inaweza kuwa kiasi kikubwa ambacho hakijawahi kushuhudiwa.

Utumiaji wa silaha aina nyingi za nyuklia unaweza kuvuruga biashara ya kimataifa na mawasiliano ya simu, redio au televisheni, intaneti na mitandao ya jamii, na pengine kusababisha kuporomoka kwa uchumi duniani, na hivyo kuzorotesha umaskini na kurudisha nyuma malengo ya maendeleo ya binadamu kwa miongo mingi.

Hakuna taifa wala mtu yeyote binafsi awezaye kujikinga na athari za silaha za nyuklia.

Hiroshima na Nagasaki

Watu zaidi ya robo milioni waliuawa wakati Marekani ilipoangusha bomu mbili za nyuklia mijini miwili ya Japan ya Hiroshima na Nagasaki mnamo Agosti 1945, ikiwa ni mara ya kwanza na ya pekee kwa silaha za nyuklia kutumika vitani.

Watu wengi walichomeka na kugeuka majivu papo hapo. Wengine walikufa kwa masumbuko makali na maumivu makubwa baada ya saa, siku au wiki kadha kufuatia mashambulizi hayo kwa kuchomeka, majeraha ya milipuko na magonjwa yaletwayo na mnururisho mkali. Wengine wasiohesabika walikufa baada ya miaka kwa kansa zinazosababishwa na mnururisho mkali, na magonjwa mengine.

Ili kuzuia kutokea tena kwa maovu kama hayo ya kikatili, ni lazima mataifa yachukue hatua za dharura za kumaliza silaha za nyuklia.

Katika Hiroshima na Nagasaki, uharibifu usio na kifani ulitokea na maafa makubwa yalifuatia na kuifanya hali ionekane kama kwamba siku ya kiyama ilikuwa imewadia: viwanja vya shule vilifunikwa na maiti za watoto, na miili ya wengine waliokaribia kufa. Akina mama walikuwa bado wameshika maiti za watoto wao wachanga. Matumbo ya watu wengine na vipande vya nyama za miili yao zilining’inia nje.

Wengi walikufa bila huduma zozote za kuwapunguzia maumivu na mateso waliyoyapata kwani ni hospitali chache zilizobaki, dawa na vifaa vingine vya matibabu ziliharibiwa, na madaktari wengi na wauguzi waliuawa ama kujeruhiwa. Waliofika katika miji hiyo kutoa misaada baada ya milipuko walikuwa wanahatarisha maisha yao kwa sababu ya masalio ya mnururisho.

Idadi kubwa ya waathiriwa – zaidi ya asilimia 90 – walikuwa ni raia, wakiwemo watoto takribani 38,000. Shambulizi la Hiroshima likitokea, wanafunzi karibu 8,400 wa shule ya upili ya daraja la chini walikuwa nje ya madarasa wakiunda fataki kama hatua ya raia kujikinga; 6,300 kati yao waliuawa.

Mabaki ya jiji la Hiroshima lililolipuliwa 1945. Picha na: Serikali ya Marekani

Onyesho mojawapo katika Hiroshima Peace Memorial Museum.

Kitovu cha milipuko

Katika kila jiji, waliokuwa karibu na kitovu cha milipuko, walikuwa na nafasi ndogo sana ya kunusurika. Karibu kila mtu aliyekuwa umbali wa ndani ya kilomita 1.2 kutoka kwenye kitovu na ambaye hakuwa amejikinga kwa vyovyote na athari za bomu alikufa papo hapo ama baada ya wiki kadhaa.

Halijoto ardhini kwenye kitovu ilifikia digrii kati ya 3,000 na 4,000 kwa vipimo vya Celsius, huku watu waliokuwa umbali wa kilomita hadi 3.5 wakipatwa na majeraha ya kuchomeka. Mitetemeko mizito iliharibu karibu majengo yote ya mbao ndani ya umbali wa kilomita mbili.

Hata katika umbali wa kilomita moja, watu waliopata kiasi kikubwa cha mnururisho unaobadilika kuwa chuma na kuingiza sumu mwilini walikufa. Watu wengi waliokuwa mbali zaidi waliaga dunia kutokana na athari za baadaye za kupatwa na mnururisho.

Athari za milipuko

Machafuko na vurumai zilizofuatia milipuko hiyo ni pamoja na wazazi waliokuwa tayari kufanya lolote wakiwatafuta watoto wao, nao watoto wakitafuta wazazi. Baadhi yao walipata tu mabaki ya mali binafsi ya wapendwa wao; wengine hawakupata chochote.

Juhudi za kukutanisha tena familia zilitatizwa na ukweli kwamba wengi walipatwa na majeraha mengi ya kuchomeka kiasi kwamba hawangetambulika kwa urahisi.

“Baada ya muda, nilichungulia nje ya makao ya kujisalimisha kutokana na mashambulizi ya mabomu kutoka angani. Niliona watu wametawanyika kote uwanjani. Uwanja karibu wote ulikuwa umefunikwa na watu. Wengi walionekana kama wamekufa kwani walitulia tuli. Hata hivyo, kulikuwa na waliokuwa wakitupatupa miguu ama kuinua mikono hapa na kule.”

– Fujio Tsujimoto, umri wa miaka mitano, Nagasaki

Baadhi ya manusura hawakuwa na majeraha yaliyoonekana lakini waliugua ghafla na kuaga dunia. Vifo vyao viliwashangaza waliofika kwanza kuwasaidia ambao hawakuwa na habari kwamba silaha mpya yenye madhara ya mnururisho ilitumika.

Wanawake wengi wajawazito katika miji hiyo walitunguliwa mimba ama wakazaa watoto waliokufa wakiwa wachanga, kwani mnururisho wa mabomu ulikuwa umeingia katika mimba. Kasoro za kuzaliwa, ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa kichwa kidogo, zikawa ni kawaida miongoni mwa watoto walioathiriwa na mabomu wakiwa ndani ya mimba za mama zao.

Nagasaki ilivyokuwa mwezi mmoja baada ya kushambuliwa. Picha na: Serikali ya Marekani

Mvulana huyu wa jiji la Nagasaki akipokea msaada wa chakula baada ya jiji hilo kushambuliwa. Picha na: Yosuke Yamahata

Baiskeli ya magurudumu matatu ya Shinichi

Hiroshima ikishambuliwa, Shinichi Tetsutani aliyekuwa na umri wa miaka mitatu alikuwa nje ya nyumba yao akifanya alichokifurahia zaidi – kuendesha baiskeli yake ya magurudumu matatu.

Alipata majeraha makubwa ikiwa ni pamoja na kuchomeka mwili wote, na aliaga dunia saa chache baadaye. Dada zake wawili, Michiko na Yoko, waliuawa pia.

Miaka mingi baadaye, baba yao alisema: “Hili halifai tena kuwatendekea watoto. Tafadhali fanyeni juhudi za kuleta amani duniani na kujenga mahala pa watoto kuchezea mpaka nyoyo zao ziridhike.”

Baiskeli ya magurudumu matatu ya Shinichi iliyochomeka imehifadhiwa katika Jumba la Makumbusho la Hiroshima Peace Memorial, na mchongo wake unapatikana katika Jumba la Makumbusho la International Red Cross na Red Crescent Museum jijini Geneva.

Imekuwa ni ishara inayotia uchungu ya mateso waliyoyapata watoto kwenye mashambulizi ya mabomu ya nyuklia.

Picha na: Jumba la Makumbusho la Hiroshima Peace Memorial Museum. Nobuo Tetsutani alilikabidhi jumba hilo baiskeli.

Dada wawili wa Hiroshima

Kimino Wataoka aliyekuwa na umri wa miaka miwili, na dadake Hirono aliyekuwa na miaka mitano, walikuwa nyumbani na wazazi wao wakati Hiroshima iliposhambuliwa. Wote wanne waliuawa.

Dada yao mwingine, Kayoko, aliyekuwa karibu na kitovu cha mlipuko, alikufa pia. Ni dadao mkubwa pekee, Chizuko, ambaye alinusurika.

Yaaminika picha hii ya Kimino (kushoto) na Hirono (kulia) ilipigwa siku moja kabla ya shambulio la bomu ya nyuklia. Picha na: Miho Iwata

Kumulikwa na miale ya bomu

Toru Ikemoto alikuwa na umri wa miaka saba, na dadake alikuwa na miaka tisa wakati Hiroshima ilipoangamizwa. Wote wawili walikuwa ndani ya nyumba yao, umbali wa karibu kilomita moja kutoka kwa kitovu cha mlipuko.

Ndani ya siku nne au tano baada ya shambulizi, nywele zao zilianza kung’oka, wakapatwa na homa na kuvuja damu kwenye ufizi – ishara za kuwa na sumu ya mnururisho mkali.

Ingawa wote wawili waliponea madhara hatari ya mwanzo mwanzo ya magonjwa, hatimaye waliaga dunia kutokana na athari za baadaye za mnururisho. Toru alikufa akiwa na umri wa miaka 11 naye Aiko akiwa na miaka 29.

Ndugu hawa wawili Toru (kushoto) na Aiko (kulia) wakiwa katika Hospitali ya Shirika la Msalaba Mwekundu ya Hiroshima mnamo Oktoba, 1945. Picha na: Shunkichi Kikuchi

Walioponea

Wale ambao, kwa bahati nzuri, walioponea kufuatia mashambulizi ya mabomu ya nyuklia katika Hiroshima na Nagasaki, walipewa jina la Kijapani ‘hibakusha’, au “watu walioathiriwa na mlipuko”.

Wengi walivumilia maumivu na usumbufu maishani yao yote kutokana na majeraha ya mwili na akili. Baadhi yao waliachwa na makovu makubwa mwilini na kwenye nyuso zao au kuishi kwa miongo wakiwa na vigae vya vioo ndani ya miili yao.

Wanawake walikabiliwa na ugumu wa kipekee na makovu ya fedheha kwa kuhofia kurithisha watoto wao na wajukuu hitilafu za kizazi zilizosababishwa na mabomu hayo.

Ndani ya miaka michache baada ya mashambulizi hayo, walionusurika walianza kuugua magonjwa ya kansa na maradhi mengine kwa kasi ya juu ambayo haikuwa ya kawaida kutokana na athari za baadaye za mnururisho. Mnamo miaka ya mwanzo, visa vya kansa ya damu (lukemia) vilikuwa kawaida.

Ili kuutahadharisha ulimwengu kuhusu hatari za silaha za nyuklia, manusura wengi wameeleza kuhusu yaliyowakumba 1945. Baadhi yao waliokuwa watoto wakati wa mashambulizi hayo wangali hai hata sasa na wameendeleza kazi ya kuueleza ukweli kuhusu madhara ya zana hizo.

Ujumbe huo umekuwa wazi na wa kutegemewa kwa miongo mingi: Binadamu na silaha za nyuklia hawawezi kuishi pamoja kwa amani.

Mnamo 2024, Nihon Hidankyo – muungano wa mashirika ya Japan yanayowakilisha manusura – lilishinda Tuzo la Amani la Nobel “kwa juhudi zake kujenga ulimwengu usio na silaha zozote za nyuklia na kwa kubainisha wazi kupitia kwa ushahidi wa manusura kuwa silaha za nyuklia hazifai kutumika tena kamwe”.

Utetezi wa kijasiri na thabiti wa manusura umewahamasisha watu wengi ulimwenguni kujiunga na wimbi la kutetea kumalizwa kwa zana za nyuklia.

Manusura na mtetezi

Mvulana wa umri wa miaka 16 kwa jina, Sumiteru Taniguchi aliponea shambulizi la bomu ya nyuklia la Nagasaki. “Mara tu nuru ya ghafula ya mlipuko ilipotokea, nilibanduliwa kutoka nyuma ya baiskeli yangu na kubwagwa chini ardhini,” akasimulia. Aliponyanyua kichwa chake, aliona watoto wote waliokuwa wakicheza karibu naye wakiwa maiti.

Ingawa alikuwa umbali wa karibu kilomita mbili kutoka kwenye kitovu cha mlipuko, alipata majeraha mabaya ya kuchomeka mgongoni, mkono wa kushoto na mguu. Muda mfupi baadaye, majeraha hayo yaliambukizwa vidudu na kuenea, na ikabidi akae hospitalini kwa karibu miaka minne akitibiwa, ikiwa ni pamoja na miezi 21 aliyolazimika kulala kifudifudi.

Uchungu kutoka kwa majeraha hayo haukuisha. Alijitolea kwa sehemu kubwa ya maisha yake kutetea kupigwa marufuku kwa silaha za nyuklia.

Sumiteru Taniguchi atazama picha yake iliyopigwa 1946, inayoonyesha makovu ya bomu la Nagasaki mgongoni wake. Picha na: Yuriko Nakao

Athari za majaribio ya nyuklia

Ili kuimarisha uharibifu na uwezo wa kuua wa nguvu za nyuklia walizonazo, na kutoa onyo kwa washindani wao, mataifa yenye silaha za nyuklia yamefanya majaribio zaidi ya 2,000 ya kulipua silaha za nyuklia kote ulimwenguni tangu 1945.

Kwa kuachilia hewani na baharini kiasi kikubwa cha mnururisho, majaribio hayo ya sumu yamesababisha majanga ya kansa na magonjwa mengine ya kudumu. Maeneo makubwa ya ardhi yangali si salama kuishi, hata baada ya miongo mingi ya kufungwa kwa maeneo ya majaribio.

Wiki tatu baada ya mashambulizi ya mabomu ya nyuklia katika Hiroshima na Nagasaki, Serikali ya Marekani ilifanya jaribio la kwanza la kulipua silaha za nyuklia katika Jimbo la New York, zoezi lililopewa jina la siri “Trinity”. Moto mkubwa kutoka kitovu cha mlipuko wa bomu uligeuza mchanga kuwa vioo, ukaangaza milima ya karibu na kurusha wingu la mabaki ya nururishi lenye umbo la uyoga umbali wa kilomita 12 hewani.

Waliokuwa wakifanya kazi katika maeneo ya majaribio na jamii jirani walipatwa na uharibifu mkubwa ambao athari zake zinaendelea kuonekana mpaka eo.

Hali imekuwa ni hiyo hiyo kwa wanaofanya kazi ama kuishi katika sehemu unakoelekea upepo na mito katika maeneo mengine zaidi ya 60 ulimwenguni ya kufanyia majaribio ya silaha za nyuklia, kuanzia jangwani za Australia na Algeria hadi maeneo makubwa yenye nyasi ya Kazakhstan na visiwa vya matumbawe vya Pacific.

Iroji Kebenli, akiwa na umri wa miaka 13 alipopata majeraha ya kuchomwa na nururishi wakati Marekani ilipofanya jaribio la silaha ya nyuklia katika Visiwa vya Marshall mnamo 1954. Picha na: Serikali ya Marekani

Wingu lenye umbo la uyoga kufuatia mlipuko wa majaribio wa bomu la nyuklia. Picha na: Serikali ya Marekani

Maeneo ya kufanyia majaribio ya silaha za nyuklia

Silaha za nyuklia zimefanyiwa majaribio katika Algeria, Australia, China, India, Kazakhstan, Kiribati, Ma’ohi Nui (French Polynesia), Visiwa vya Marshall, Korea Kaskazini, Pakistan, Russia, Turkmenistan, Ukraine, Marekani na Uzbekistan.

Majaribio ya kulipua silaha za nyuklia angani – ikiwa ni pamoja na 500 yaliyofanyika kuanzia 1945 hadi 1980 – yalikuwa hasa na athari mbaya, yakasambaza chembe nururishi mbali na katika sehemu pana. Silaha zote hizo zikiunganishwa zilikuwa na uwezo wa kuharibu ulio sawa na wa mabomu 29,000 ya nyuklia kama lililongushwa Hiroshima.

Hivi leo, kila mtu aliye hai anabeba ndani ya mwili wake chembe nururishi kutoka kwa majaribio yanayofanywa angani na hivyo kuongeza hatari ya magonjwa. Madaktari wa matibabu wanabashiri kwamba baada ya muda, majaribio yaliyopita yatasababisha vifo vya mapema visivyopungua milioni nne kutokana na kansa na magonjwa mengine.

Majaribio ya kulipua silaha za nyuklia baharini na chini ya ardhi yamekuwa pia na madhara ya muda mrefu kwa afya na mazingira.

Kwa kujali kuhusu athari za majaribio ya silaha za nyuklia ulimwenguni, maandamano makubwa katika sehemu nyingi za dunia yalifanyika mwisho mwisho wa nusu ya kwanza ya karne ya 20. Maandamano hayo yalilazimisha viongozi kushauriana kuhusu upigaji marufuku kwa kiasi wa silaha hizo mnamo 1963. Uharamishaji kamili mnamo 1996 ulifuatia. Hatua hizo mbili zimesaidia kuzuia majaribio ya silaha za nyuklia ulimwenguni.

Lakini athari za majaribio ya mapema kwa maisha ya watu na mazingira dhaifu zitaendelea kuonekana kwa vizazi vijavyo. Jamii ya kimataifa ina jukumu sio tu la kuhakikisha kwamba uharibifu kama huo hautokei tena lakini kujitahidi pia kuakisi madhara yaliyotendeka.

Manusura wachache wa majaribio ya silaha za nyuklia popote ulimwenguni wamefidiwa kwa mateso yao, na juhudi za kusafisha maeneo ya zamani ya kufanyia majaribio hazitoshi. Katika baadhi ya maeneo, maporomoko ya majengo na miundo msingi mingine ni hatari inayoendelea ya utoaji sumu zaidi.

Mlipuko wa majaribio uliofanywa 1971 na Ufaransa katika Moruroa Atoll iliyomo Ma’ohi Nui. Picha na: Serikali ya Ufaransa

Shimo la katikati ya mlima lililochimbuliwa na mlipuko wa jaribio la bomu la nyuklia lililofanywa na Russia katika Kazakhstan. Picha na: CTBTO

Ubaguzi wa jamii za asili katika majaribio ya silaha za nyuklia

Imani zinazoegemea ubaguzi kulingana na asili za watu zimeendelea kuzingatiwa katika kufikia maamuzi ya kufanya majaribio ya silaha za nyuklia, huku serikali na waliokatalia mawazo ya nguvu za kikoloni wakiendelea kuamini kuwa watu wa asili wanaweza kutolewa mhanga, na ardhi zao takatifu hazina thamani na ni za mbali.

“Ardhi yetu, bahari yetu, jamii zetu na miili yetu zinabeba ‘urithi’ wa majaribio hayo hatari sasa na kwa vizazi vijavyo visivyojulikana,” akasimulia Karina Lester, mwanamke wa jamii ya Yankunytjatjara Anangu kutoka Australia, kwa niaba ya makundi ya jamii asili, akitoa ushahidi katika kikao cha Umoja wa Mataifa mnamo 2017.

Kwenye harakati za kutafuta “silaha hatari zaidi zenye uwezo wa kusababisha uharibifu mkubwa na maafa mengi” wenye mamlaka wameendelea kuwatendea watu wa jamii za asili sawa ‘nungubandia’ kwa kuwatumia kwa majaribio, akasema. Ni nadra sana kwao kuombwa kibali, sembuse kutakiwa kutoa idhini, na walipewa kiasi kidogo au kunyimwa kinga kabisa.

Urithi wa sumu wa majaribio ya silaha za nyuklia umepokonya jamii nyingi uhusiano na maisha yao ya kitamaduni, hawawezi kurudi katika maeneo yao takatifu ya mababu zao ama kujipatia riziki kutoka kwa ardhi zao, mito na bahari, kama ambavyo wamekuwa wakifanya kwa karne nyingi.

Australia: Kupokonywa uwezo wa kuona na bomu

Mnamo 1953, wakati Yami Lester akiwa na umri wa miaka 10, Uingereza ilianza kufanya majaribio ya silaha za nyuklia katika Emu Field karibu na nyumbani kwao, sehemu ya mbali na miji ya Australia.

Anaikumbuka takataka ya nururishi, au ‘ukungu mweusi’ ikiifunika anga. Ukungu huo uIiwasha macho yake na miaka minne baadaye, alikuwa amepoteza kabisa uwezo wa kuona.

“Nilikuwa ninacheza na watoto wengine. Ni wakati huo ambapo bomu lililipuka.” Akavuta kumbukizi. “Ninaikumbuka sauti iliyotokea, ilikuwa sauti isiyo ya kawaida, haikuwa ya juu, sio kama sauti ambayo nimewahi kusikia awali. Wakati huo huo ardhi ilitetemeshwa na tungehisi sehemu yote ikisonga.”

Saa kadhaa baadaye, kila mtu katika jamii yake alianza kuugua. “Sote tulikuwa tunatapika; tukaharisha, ngozi zikatuwasha, na macho yakauma,” akasema. “Baadhi ya wazee miongoni mwetu walikufa.”

Hatimaye, Yami akawa mtetezi wa watu asili ya Australia walioathiriwa na majaribio hayo. Hata baada ya kifo chake 2017, watoto wake wameendeleza juhudi zake kutetea haki.

Picha na: Jesse Boylan

Kazakhstan: Msanii aliyezaliwa bila mikono

Karipbek Kuyukov alikulia kijijini Yegyndybulak, karibu na Semipalatinsk, Kazakhstan – eneo kubwa zaidi la Urusi la majaribio ya silaha za nyuklia. Anakumbuka akiwa mtoto vile fanicha, vyungu, vikombe na sahani zilitetemeka kila mara mlipuko wa jaribio la bomu la nyuklia ukitokea.

Kabla hajazaliwa, wazazi wake walizoea kwenda juu ya kilima cha karibu na nyumbani kwao ili kujionea vizuri wingu kubwa angavu lenye umbo sawa na uyoga likipaa juu angani.

“Hawakujua kuhusu hatari zilizokabili afya zao na athari angamizi za jinai waliyokuwa wakifanyiwa,” akakumbuka.

Karipbek alizaliwa 1968 bila mikono. Lakini hilo halikumzuia kuibuika kuwa msanii msifika anayetumia miguu yake na mdomo kuchora kwa rangi. Ujumbe mkuu wa kazi zake za sanaa ni kupinga utumiaji wa silaha za nyuklia.

“Kazi yangu maalumu katika ardhi hii ni kufanya kila niwezalo kwa watu walio kama mimi kuwa wahanga wa mwisho wa majaribio ya silaha za nyuklia,” akasema. “Sitaki majaribio hayo yafanyike tena popote au wakati wowote, na kokote katika dunia hii … Anga na ibaki ikiwa safi na watoto wetu wawe na afya nzuri!”

Kuanzia 1949 hadi 1989, Urusi ilifanya majaribio zaidi ya 450 ya mabomu ya nyuklia katika Semipalatinsk, karibu robo ya majaribio yote yaliyofanyika ulimwenguni.

Mojawapo ya kazi za sanaa za Karipbek Kuyukov, inayoitwa “Fear”.

Visiwa vya Marshall: Utawala wa nururishi

Nerje Joseph alikuwa na umri wa miaka saba mnamo 1954 wakati Marekani ilipofanya jaribio lake kubwa zaidi la kulipua bomu la nyuklia katika zoezi chapa “Castle Bravo”, umbali wa kilomita 160 kutoka nyumbani kwake, Rongelap Atoll, ndani ya Visiwa vya Marshall.

Mlipuko huo ulikuwa mkubwa kuliko ilivyotarajiwa na ulisababisha kuenea kwa sumu zaidi. Anga ilibadilika kuwa rangi ya chungwa kisha waridi. Hakuna yeyote miongoni mwa wenyeji wa kisiwa hicho cha matumbawe aliyefahamu kilichofanyika.

Saa kadhaa baadaye, majivu nururishi na vipande vya matumbawe zikaanza kunyeshea nyumba zao, zikachafua ngozi zao, maji na chakula. Muda mfupi baadaye wakaanza kupata ishara za magonjwa yaletwayo na mnururisho uliopita kiasi.

Nywele zote za Nerje ziling’oka, na sawa na karibu kila mtu kisiwani, akapata majeraha ya kuchomeka mwilini.

Siku kadhaa baadaye, wenye mamlaka kutoka Marekani waliwahamisha wakazi wa Rongelap na kuwapeleka kisiwani kingine cha matumbawe kwa sababu ya hatari kubwa kwa afya zao kutokana na cheche za mnururisho kufuatia mlipuko wa bomu la nyuklia. Lakini miaka mitatu baada ya kuhamishwa, wakuu hao wa Marekani waliwahimiza kurudi Rongelap, kwani walitaka kuchunguza madhara ya afya ambayo yangesababishwa na mabaki ya mnururisho.

“Data ya aina hiyo haijawahi kupatikana,” akasema afisa mmoja wa Marekani wakati huo. “Ingawa watu hawa hawaishi kama watu wastaarabu wa nchi za magharibi, ni kweli kwamba wanakaribia sana kufanana nasi, tofauti kabisa na panya.”

Uamuzi wa kuwarudisha Rongelap wanakisiwa hao uliwaletea balaa. Walikumbana na ongezeko la aina tofauti za kansa, mimba kuharibika, watoto kuzaliwa wakiwa wafu na wengine wakiwa na dosari za kimaumbile.

Kutokana na mkusanyiko wa chembe za mnururisho zenye uzito tofauti na chembe nyingine, ikawa ni lazima Nerje afanyiwe upasuaji kuondoa kikoromeo chake. Alitamani warejelee siku za zamani za furaha kabla majaribio ya silaha za nyuklia hayajafanyika.

Kati ya 1946 na 1958, Marekani ilikuwa imefanya majaribio 67 ya kulipua mabomu ya nyuklia katika Visiwa vya Marshall. Jaribio la Castle Bravo pekee lilisababisha mlipuko uliokuwa na uzito mara 1,000 ukilinganishwa na wa bomu la Hiroshima.

Mpaka wa leo, visiwa vingi vya matumbawe si salama kwa binadamu kuishi, wala kuendesha shughuli za kilimo au uvuvi.

Nerje Joseph aonyesha upara aliopata baada ya nywele zake  kung’oka, pamoja na majeraha ya kuchomeka miguu kutokana na nururishi. Picha na: Serikali ya Marekani

Vianzo vingine vya madhara

Vipengele vingine vya uundaji wa silaha za nyuklia – kuanzia uchimbaji wa madini ya urani hadi utupaji wa taka za mnururisho – vina madhara haribifu pia kwa afya ya binadamu na mazingira.

Kwenye migodi ya urani – ambapo utaratibu wa kuunda silaha za nyuklia unaanzia – uchafuzi wa nururishi na kemikali kutokana na mabaki ya takataka hupenya mchangani na njia za kupitia maji, unaathiri wafanyakazi na jamii za karibu. Hakuna mgodi popote duniani ambapo takakata zimeondolewa baada ya uchimbaji kumalizika.

Uchafuzi wa nururishi umetokea pia katika tanuri za nyuklia ambazo hutumika kutengeneza chembe za silaha za nyuklia. Kiwanda cha nishati ya nyuklia cha Windscale, Uingereza, kilichomeka kwa siku tatu mnamo 1957 na kurusha nyoya za mnururisho katika maeneo mengi ya Ulaya. Maziwa yote ya ng’ombe kutoka mashambani ya karibu yaliharibiwa.

Jamii nyingi ulimwenguni hukabiliwa pia na changamoto zisizoisha zinazohusiana na uhifadhi salama wa kiasi kikubwa cha takataka za nyuklia zilizokusanywa kutoka kwa uundaji wa makumi ya maelfu ya silaha za nyuklia tangu 1945. Takataka hiyo itabaki kuwa hatari kwa miaka mingine maelfu.

Waandamanaji wanaopinga uundaji na utumiaji wa silaha za nyuklia katika Jimbo la Arizona, Marekani. Picha na: Jack Cohen-Joppa

Silaha za nyuklia zilizopo

Hivi leo, mataifa tisa yana maelfu kadhaa ya silaha za nyuklia, hali ambayo ni tisho la kipekee kwa maisha ya binadamu popote. Mamia ya silaha hizo huwekwa katika tahadhari ya kiwango cha hali ya juu, tayari kutumika ndani ya dakika chache.

Zinahifadhiwa katika vituo vya kurushia makombora, ndani ya ndege za kivita na manowari zinazoweka doria baharini nyakati zote. Baadhi yake zinaweza kusafiri umbali wa maelfu ya kilomita kupitia mabara ili kufikia zinakolengwa.

Ukweli: Mataifa tisa ulimwenguni ambayo yanamiliki silaha za nyuklia yana takribani silaha [FACT]fact-nuclear-weapons[/FACT].

Mengi ya mataifa hayo yana mabomu yawezayo kusababisha uharibu mkubwa na maafa mengi kuliko mabomu yaliyoangushwa Hiroshima na Nagasaki katika mwanzo wa enzi ya utumiaji wa silaha za nyuklia. Mabomuma kubwa zaidi yana nguvu za zaidi ya tani milioni moja, au megaton moja, ya kemikali ya kisasi inayolipuka, TNT.

Hata mabomu yanayokusudiwa kutumika katika harakati za kivita, yanaweza kusababisha mlipuko wenye nguvu mara 20 zaidi ya bomu lililoangushwa Hiroshima.

Manowari moja yenye silaha za nyuklia inaweza kubeba makombora dazeni moja au zaidi, kila moja ikiwa na kichwa cha nyuklia, yenye uwezo wa pamoja wa kuharibu miji zaidi ya 100.

Mataifa yenye silaha za nyuklia

Mataifa tisa yana silaha za nyuklia hivi leo: Marekani, Russia, China, Ufaransa, Uingereza, India, Pakistan, Israeli na Korea Kaskazini. Russia na Marekani ndizo zina hifadhi kubwa zaidi ya silaha za nyuklia.

Watu wanaoishi karibu na kambi za kijeshi zinazotumika kurushia silaha za nyuklia hukabiliwa na hatari kubwa ya kuwa waathiriwa wa mashambulizi ya kinyuklia, ama kupata hasara kutokana na milipuko ya nyuklia iwezayo kutokea kimakosa na kwa bahati mbaya. Kwa vile mambo mengi ya serikali huwekwa siri, huenda baadhi ya watu karibu na kambi hizo hawana habari kuhusu kuwepo kwa silaha karibu nao.

Nyingi ya silaha hizo haziwekwi tu katika maghala. Hutolewa kila mara, tayari kutumiwa wakati wowote. Serikali huhusika katika miradi inayogharimu pesa nyingi ya kuimarisha na kupanua hifadhi zao, kwa kisingizio cha kupata zana za kisasa.

Baadhi ya mataifa yenye silaha za nyuklia yanatengeneza aina mpya ya silaha hizo, yanafanyia majaribio mifumo mipya ya kuzitumia na kueneza nadharia za uwezakano wa kutumia silaha hizo. Yaonekana lengo la mataifa hayo yote ni kuendelea kudumisha nguvu zao za nyuklia kwa hali ya baadaye isiyojulikana itakavyokuwa.

Kombora la nyuklia la Russia laonyeshwa katika gwaride la kijeshi lililofanyika 2023. Picha na: Serikali ya Russia

Makombora ya nyuklia ya Marekani yakionyeshwa katika jumba la makumbusho. Picha na: Serikali ya Marekani

Mataifa yanayokula njama za kudumisha silaha za nyuklia

Ingawa ni mataifa tisa yenye silaha za nyuklia, mengine zaidi ya 30 yanaunga mkono kubakizwa kwa silaha hizo na uwezekano wa kuzitumia, ikiwa ni pamoja na madai ya kulindwa na ‘mwavuli wa kinyuklia’ wa nchi marafiki zenye hifadhi za nyuklia.

Kwa mfano, mataifa yote wanachama wa Umoja wa Kujihami wa Nchi za Ulaya (NATO), yameidhinisha hadharani silaha za nyuklia. Baadhi yao yameipatia Marekani hifadhi ya mabomu ya nyuklia katika nchi zao – ikiwa ni pamoja na Ubelgiji, Ujerumani, Italia, Uholanzi na Türkiye – na kutoa ndege na watu wanaohitajika kuziangusha. Belarus inahifadhi silaha za Russia.

Baadhi ya mataifa hubadilishana ripoti za kijasusi kwa shabaha ya kuamua panapohitaji kulengwa kwa silaha za nyuklia, ama kuruhusu meli zenye silaha za nyuklia kupitia baharini zao na kutia nanga bandarini zao au ndege zenye silaha za nyuklia kuingia anga ya nchi hizo na kuongezwa mafuta katika viwanja vyao vyao ndege.

Matendo yote hayo ya kula njama huendeleza hatari za silaha za nyuklia na kudhoofisha juhudi za kumaliza silaha hizo.

Waandamanaji katika Ujerumani waziba lango la kambi ya kijeshi inayohifadhi mabomu ya nyuklia ya Marekani. Picha na: Ralf Schlesener

Wasiwasi kuhusu ueneaji

Kukataa kwa nchi zenye silaha za nyuklia kupunguza na hatimaye kumaliza zana hizo kumeimarisha hatari ya mataifa zaidi, na hata wahusika ambao si serikali, kupata silaha za nyuklia siku moja. Kupiga hatua katika upunguzaji wa silaha hizo ni hali muhimu ya kuzuia kuenea kwake.

Ingawa hatua muhimu zimechukuliwa kuzuia ueneaji wa silaha hizo, hakuna uhakika kwamba zitaleta matokeo yanayotakiwa. Taifa lolote lenye uwezo wa urani au kutayarisha upya mafuta ya nyuklia ili kutoa plutoni linaweza, kwa kudhania tu, kuunda silaha ya nyuklia ndani ya miezi kadhaa.

Afrika Kusini, Israeli, India, Pakistan na Korea Kaskini zilijipatia silaha za nyuklia kwa kutumia vifaa na nyenzo zilizodaiwa kulenga amani, na hivyo kukariri hatari za kuendelea kuongezwa kwa silaha hizo chini ya mipango ya nguvu za nyuklia.

Kilo kadhaa za urani iliyostawishwa au kemikali ya plutoni zinatosha kuunda bomu moja la nyuklia. Hivi leo, mamia ya tani za nyenzo hizo zimewekwa akiba ulimwenguni, na nyingine nyingi bado zinaundwa. Ni lazima tatizo hilo lishughulikiwe Ili kufanikisha upunguzaji wa silaha hizo za vita.

Kutetea marufuku

Ili kulinda wanadamu kutokana na maangamizi na madhara yasiyogeuzika ya silaha za nyuklia, serikali hazina budi kuchukua hatua za dharura ili kumaliza zana hizo.

Makumi ya maelfu ya silaha za nyuklia yameharibiwa katika kuitikia miito ya watu kutoka kote duniani wakihimiza upigaji marufuku wa silaha hizo. Afrika Kusini ndiyo nchi pekee ambayo imemaliza kabisa silaha za nyuklia; nchi nyingine dazeni kadhaa zimetupilia mbali mipango ya kujipatia silaha hizo.

Vita ya maneno na propaganda kati ya nchi za Magharibi na Mashariki ikiwa kileleni, kulikuwa na silaha takribani 70,000 za nyuklia. Upunguzaji mkubwa wa silaha hizo duniani ulitokea katikati ya miaka ya 1980 na mapema 2000.

Lakini katika siku za karibuni, miradi ya kupunguza mabomu ya nyuklia imekwama, huku baadhi ya mataifa yenye silaha za nyuklia yakiongeza hifadhi yake kwa kasi ya kipekee. Hakuna hata mojawapo ya mataifa hayo limetangaza mpango wa kumaliza silaha hizo kabisa.

Hata hivyo, mataifa mengi ya ulimwengu yanapinga vikali silaha za nyuklia na yanataka zimalizwe mara moja.

Haitoshi kukomesha ueneaji wa silaha hizo katika mataifa zaidi, ama kuweka masharti kuhusu hali ambapo zinafaa kutumiwa. Ikitiliwa maanani kuwa silaha hizo ni hatari kubwa kwa maisha yote katika dunia yetu, suluhisho la pekee ni kuzipiga marufuku.

Hifadhi ya Wasanii wanopinga Mabomu. Picha na: Miki Anagrius

Si adilifu, ni haramu na kinyume na misingi ya kidemokrasia

Silaha za nyuklia husababisha maafa mengi na uharibifu mkubwa, na ni tisho kubwa kwa maisha ya binadamu. Mauaji ya kiholela na kulemazwa kwa mamia ya maelfu ya watu hazina msingi wowote wa uadilifu.

Utumiaji wowote wa silaha za nyuklia unafaa kuwa ni kinyume cha sheria za kimataifa na uchukuliwe kuwa kosa kubwa la uhalifu wa kivita. Silaha zozote ziletazo maangamizi haziwezi kuwa na matumizi halali ya kijeshi au vitani.

Kura za maoni kote ulimwenguni, ikiwa ni pamoja na nchini zenye silaha za nyuklia, zinaonyesha kuungwa mkono na wengi kwa marufuku ya silaha hizo. Serikali zinazoendelea kuunda silaha za nyuklia zinafanya hivyo kinyume kabisa na mapenzi ya raia wake.

Kila mtu, popote alipo, atanufaika kutokana na kumalizwa kwa silaha hizo za kuogofya.

Hatari inayozidi kuongezeka ya kutumia silaha za nyuklia

Bado pana hatari kubwa ya kutumia silaha za nyuklia hata leo, iwe ni kimakosa au makusudi. Inaonekana kana kwamba hatari hiyo inazidi kuongezeka.

Hali hiyo inatokana na vitisho vinavyokabili mazingira ya usalama wa kimataifa, kuongezeka kwa mivutano miongoni mwa mataifa yenye silaha za nyuklia, mataifa hayo kuendelea kuongeza silaha zao za nyuklia, na kuzorota kwa kanuni na asasi za kimataifa.

Tishio hilo linazidishwa na harakati za kuimarisha uchokozi kupitia kwa saiba, teknolojia zinazopatia watumiaji uwezo wa kujitawala, na utumiaji wa akili mnemba (AI) katika shughuli za majeshi.

Kuweka silaha za nyuklia katika hali ya juu ya tahadhari – tayari kutumiwa ndani ya dakika chache baada ya kuonywa kuhusu uwezekano wa shambulio kutokea – ni mazoea hatari zaidi. Kombora la nyuklia likirushwa hewani, haliweza kurudishwa. Ni lazima lisafiri hadi kufikia lengo lake, hata kama lilirushwa kufuatia habari zisizo za kweli.

Viongozi wanapogubikwa na ukungu wa vita, wanaweza kuchukua hatua zisizotabirika wala bila sababu. Uwezekano wa kutoelewana huwa kubwa, hasa katika hali ya dhiki na vurugu.

Ndiposa inakuwa ni rahisi kubashiri jinsi kipindi cha hofu kubwa ya ghafla au cha kukosa huruma, kitendo cha kuudhi nafsi au kupokea habari za kupotosha zinaweza kuletea ulimwengu maangamizi, kwani uwezo wa kusababisha madhara na maafa makubwa ulimwenguni umo mikononi mwa watu wachache.

Kwa mara nyingi wakati wa vita ya maneno na propaganda kati ya mataifa ya Magharibi na Mashariki, ulimwengu ulikaribia sana kujipata vitani kamili ya nyuklia. Upeo wenye sifa mbaya ulitokea 1962 wakati wa mgogoro wa makombora ya Cuba uliohusu Marekani na Urusi.

Ingawa ni kweli kwamba silaha za nyuklia hazijawahi kutumika vitani tangu 1945, hali hiyo imetokana na bahati tu wala sio usimamizi mwema. Na huenda karibuni, tusiwe tena na bahati hiyo iwapo hatua thabiti hazitachukuliwa kumaliza tisho hilo.

Kuzuia nyuklia

Mara nyingi mataifa yenye silaha za nyuklia hutumia kisingizio cha kuzuia silaha zaidi za nyuklia kuundwa na kuenezwa kama sababu ya kuendelea kudumisha hifadhi zao za silaha hizo. Yanadai sababu kuu ya kuwa na zana hizo ni kuzuia mataifa mengine kuanza mashambulizi ya nyuklia, na hivyo yanachangia amani na utulivu duniani.

Lakini mataifa mengi hayakubaliani na kauli hiyo na yanaonelea kuwa uamuzi wa mataifa hayo kuhifadhi silaha za nyuklia kwa madai ya kuzuia mataifa mengine kuunda na kueneza silaha hizo ni mwelekeo hatari, potovu na usio endelevu kwa masuala ya usalama. Isitoshe, ni tendo la kuendeleza uchokozi kutokana na wasiwasi wao wa kila mara na wanaouamini, na hivyo kuwapatia sababu ya kusababisha maafa mengi na uharibifu mkubwa.

Kinyume na madai ya wanaounga kuzuia uundaji na uenezaji zaidi wa silaha za nyuklia, kuwepo kwa silaha hizo duniani hakujazuia migogoro, ikiwa ni pamoja na matendo ya kuzichokoza nchi zenye silaha za nyuklia. Ukweli ni kwamba uwezekano wa mapigano na makabiliano umezidishwa na ongezeko la mivutano, vitisho na usaliti.

Dhana ya kuzuia nchi zisizo na silaha za nyuklia kuziunda, kuzieneza na kuzitumia inapendekeza kwamba mataifa yenye silaha hizo yana sababu halali na zana hizo ni chanzo cha kufaa cha usalama. Kauli hii huhimiza ongezeko na kuzuia upunguzaji wa silaha za nyuklia.

Ajali na makosa

Isipokuwa tisho la kutumia makusudi silaha za nyuklia, huwa kuna hatari ya zana hizo kulipuliwa kimakosa, kutokana na matatizo ya mitambo, shambulio la saiba, kuelewa vibaya onyo ama mtu asiyeruhusiwa akiingia kwenye mitambo ya uthibiti na usimamizi.

Ajali nyingi za silaha za nyuklia ambazo zimetokea tangu 1945, ikiwa ni pamoja na matukio ambapo nusura silaha hizo zitumike kimakosa, ni thibitisho la hatari kubwa iwezayo kutokea na kusababisha balaa isiyokusudiwa.

Kwa mfano, mnamo 1968, ndege ya Marekani iliyokuwa imebeba mabomu manne ya nyuklia ilishika moto na kuanguka karibu na Greenland, ikachafua eneo ambapo ilianguka kwa kemikali ya plutoni. Kwa bahati nzuri, hakukuwa na mlipuko na hivyo eneo likaepuka athari za nyuklia.

Mnamo 1995, maafisa wa Russia walishuku kuwa roketi ya utafiti wa kisayansi iliyorushwa na Norway ilikuwa kombora la Marekani kutoka kwa manowari. Kiongozi wa Russia alipewa alama za siri ambazo angetumia kwa shambulio la kulipiza kisasi lakini hatimaye akathibitisha kuwa wasiwasi wao haukuwa na msingi.

Visa vingine vya kuhofisha vimehusu kupotea kwa silaha za nyuklia baharini, manowari zenye silaha za nyuklia kugongana, na kudhania mbayuwayu wakipaa angani ama nuru inayorudishwa kutoka angani ni makombora ya nyuklia, na kuweka kimakosa kanda za mafunzo katika kompiuta za kufanyia kazi na hivyo kuigiza shambulio linaloingia la nyuklia.

Mwaka 1961, mabomu mawili ya nyuklia yaliangushwa katika Jimbo la Carolina Kaskazini la Marekani wakati ndege iliyoyabeba ilipopoteza bawa. “Kwa chembe ndogo ya bahati, kukatika kwa waya mbili kuliepusha mlipuko wa nyuklia,” akasema Robert McNamara, Waziri wa Ulinzi wa Amerika wakati huo. Picha na: Serikali ya Marekani

Kukwamisha shughuli za ufadhili

Utumiaji wa hata silaha moja ya nyuklia popote ulimwenguni unaweza kutatiza huduma za afya na muundo msingi wake, na hivyo kukwamisha shughuli za ufadhili.

Hospitali na watoaji wa dawa, vifaa vya kuzima moto, mifumo ya mawasiliano na usafiri itabaki kuwa vifusi kote katika sehemu za umbali wa kilomita kadhaa zilizoharibiwa kabisa.

Wanaothubutu kujaribu kuwasaidia wagonjwa na majeruhi huhatarisha maisha yao kutokana na kiasi kikubwa cha unururifu.

Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limekuwa likionya kila mara kuwa hakuna uwezo kamili wa kuendeleza shughuli za ufadhili na kutoa misaada hitajika silaha moja ya nyuklia ikitumika kufanya shambulizi, na hakuna uwezekano wa kuwahi kuujenga mfumo kamili wa ufadhili na misaada hitajika.

Kadhalika, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), limefikia uamuzi kuwa: “Huduma za matibabu zilizosalia haziwezi kupunguza ukali au uzito wa maafa kutokana na silaha za nyuklia kwa njia yoyote ya maana.”

Manusura mmoja wa Hiroshima aonyesha kwa mchoro kituo kimoja cha misaada jijini hilo mnamo 1945. Majeruhi walikufa mmoja baada ya mwingine. Picha na: Fumiko Yamaoka

Je, mahandaki yanaweza kusaidia?

Kujenga mahandaki zaidi ya kujikinga na athari za milipuko ya nyuklia, ama hifadhi za kujilinda na cheche za mnururisho zinazotokana na milipuko ya nyuklia, si ufumbuzi wa tatizo. Mahandaki na hifadhi hizo zilipamba moto wakati wa vita ya maneno na propaganda katika ya nchi za Magharibi na Mashariki, na kuwapatia raia matumaini yasiyo na msingi ya uwezekano wa kuendelea kuishi hata vita ya nyuklia ikitokea.

Shambulio la bomu la nyuklia likitokea, hakuna uhakika kwamba kuna mtu atakuwa na taarifa za awali kulihusu, hivyo basi hapatakuwa na nafasi ya kujisalimisha.

Isitoshe, mahandaki mengi karibu na ardhi kwenye kitovu cha mlipuko huenda yakageuka kuwa tanuu za joto na hivyo kuua kila mtu aliye ndani. Ukweli ni kwamba baadhi ya silaha za nyuklia zimeundwa kupenya ndani chini ya ardhi ili kuharibu mahandaki.

Wanaofanikiwa kupata mahandaki mapema na kuponea wakiwa ndani, wanaweza kukabiliwa na hali ya hatari isiyopendeza ya kupambana na nururishi wakitoka nje, na nafasi ya kuokolewa ni ndogo sana.

Uharibifu wa rasilmali

Kila mwaka, mataifa yenye silaha za nyuklia hutumia mabilioni mengi ya dola kuimarisha na kupanua uwezo wao wa nyuklia – pesa ambazo zingewekezwa katika huduma za afya, elimu, miradi ya kukabiliana na umaskini na hatua za kushughulikia wasiwasi mkubwa unaotokana na hali ya anga.

Katika baadhi ya mataifa, mashirika hujipatia faida kubwa kwa kuunga mkono na kufadhili ustawishaji na utengenezaji wa silaha za nyuklia. Jumuiya za washauri mabingwa na vyuo vikuu pia huhusika na hufaidika kifedha.

Kukomesha shughuli hizo za kuleta maafa kunaweza kuhakikisha rasilmali zinaelekezwa kwa mipango mingine na kuruhusu baadhi ya wataalamu wepevu wa kisayansi kuchangia katika kuujenga ulimwengu wenye amani zaidi – badala ya kuimarisha uwezo wa majeshi yao kuua na kusababisha uharibifu mkubwa.

Manowari yenye silaha za nyuklia ikiundiwa Uingereza. Picha na: Serikali ya Uingereza

Pingamizi kwa amani

Silaha za nyuklia hazichangii chochote katika kushughulikia changamoto zozote zilizopo za usalama. Badala yake, zinazorotesha hali na hata kuwa chanzo kikuu cha changamoto hizo.

Ulimwengu ukifanikiwa kumaliza silaha za nyuklia, upatanifu na uhusiano mwema miongoni mwa mataifa utaimarika na hivyo kutoa nafasi ya kuinua ushirikiano wa kimataifa kwa manufaa ya watu kila mahali – ikiwa ni pamoja na katika mataifa yanayomiliki silaha za nyuklia.

Hatua hivyo, itakuwa ni kwa manufaa makubwa ya raia wa ulimwengu, na kuyafaa maslahi ya kitaifa na ya pamoja ya usalama.

Tahakiki ya jinsia

Mara nyingi viongozi ambao hutangaza kuwa tayari kutumia silaha za nyuklia hupongezwa wakitajwa kuwa wanaume dume, hodari na wenye uwezo wa kuamua. Kwa upande mwingine, wanaounga mkono kupunguzwa na hatimaye kumalizwa kabisa kwa silaha hizo hupuuziliwa mbali wakitajwa kuwa na tabia za kike, wadhaifu na wenye kuongozwa na mhemuko.

Isitoshe, mijadala ya umma na maamuzi kuhusu silaha za nyuklia mara nyingi hutawaliwa na wanaume.

Kwa kupigana kikamilifu na dhana hizo na kuhakikisha ushirikishwaji zaidi wa jinsia zote, pana uwezekano mkubwa wa kufanikiwa kwa harakati za kupunguza na hatimaye kumaliza silaha za nyuklia.

Marufuku ya silaha za nyuklia

Mnamo 2017, baada ya mwongo mmoja wa utetezi ulioongozwa na shirika la Kampeni ya Kimataifa ya Kukomesha Silaha za Nyuklia (ICAN) na washirika wake, mataifa 122 yalipitisha kauli ya kuuidhinisha mkataba wa kihistoria wa kupiga marufuku silaha mbaya zaidi ulimwenguni, Mkataba Kupiga Marufuku Silaha za Nyuklia (TPNW), ambao ulianza kutekelezwa 2021.

Kabla ya mkataba huo kuidhinishwa, silaha za nyuklia ndizo zana pekee ambazo hazikuwa chini ya marufuku pana ulimwenguni ya silaha za kusababisha maangamizi makubwa. Mkataba huo mpya ulijaza pengo kubwa katika sheria ya kimataifa.

Chimbuko la mkataba ni wasiwasi mkubwa kutokana na tisho la hatari inayozidi kuongezeka ya silaha za nyuklia kwa maisha ya binadamu, mazingira, ustawi wa jamii na uchumi, uchumi wa kimataifa na afya na maslahi ya vizazi vilivyopo na vijavyo.

Haukuwa tu mkataba wa kwanza wa kimataifa kupiga marufuku silaha za nyuklia lakini ni wa kwanza kutoa mifumo ya kuthibitisha kumalizwa kwa silaha za nyuklia na kuwasaidia waathiriwa wa matumizi na majaribio yake.

Ukweli: Kufikia sasa, mataifa [FACT]fact-ratifications[/FACT] yameidhinisha na kuuridhia Mkataba wa Kupiga Marufuku Silaha za Nyuklia, huku mataifa mengine [FACT]fact-signatories[/FACT] yakisaini. Zaidi yanapaswa kufuata mwongozo wao.

Ingawa kufikia sasa hakuna taifa lolote lenye silaha za nyuklia ambalo limeyaridhia makubaliano ya TPNW, mkataba huo unabaki kuwa ala ya msingi ya kuimarisha mwiko wa kimataifa kuhusu utumiaji wa silaha za nyuklia na kusukuma hatua zilizopitiliza muda mrefu za kupunguza na hatimaye kumaliza silaha hizo.

Historia imethibitisha kuwa kupiga marufuku aina fulani za silaha hufanikisha hatua za kuzikomesha zana hizo. Silaha zilizopigwa marufuku zinazidi kuonekana kuwa haramu na hivyo basi kupoteza hadhi yake ya kisiasa na pia rasilmali za kuzitengeneza.

 

“Ilikuwa ni hatua ya kipekee kuanza kuutekeleza Mkataba wa Kupiga Marufuku Silaha za Nyuklia mnamo Januari, 2021, na hatimaye kuelekea kumalizwa kabisa kwa silaha za nyuklia.”

– António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, 2021

Kadiri mataifa zaidi yanavyojiunga na TPNW muda unavyoendelea, ndivyo kanuni na matakwa yake zitaimarika, na kuzidisha shinikizo kwa mataifa yenye silaha za nyuklia kukubali kanuni zake. Kufikia sasa, zaidi ya nusu ya mataifa ya ulimwenguni yamejiunga na mkataba huo.

Mkataba wa TPNW unatoa fursa yenye nguvu kwa ulimwengu kuchagua njia mbadala ya kuepuka kubaki ukitawaliwa na vitisho vya maangamizi makubwa ya nyuklia. Unatoa nafasi ya kuendelea mbele wakati ambapo tumefikia upeo wa hali ya wasiwasi mkubwa unaotia hofu.

Sherehe ya maafisa wa ngazi za juu ya kutia sahihi mkataba wa TPNW mnamo 2017. Picha na: Umoja wa Mataifa UN Photo

Kanuni kuu za TPNW

Makatazo

Mkataba wa TPNW unayakataza mataifa kutothubutu kamwe kustawisha, kufanya majaribio, kutengeneza, kupata, kuhifadhi, kuhamisha, kutumia au kutisha kutumia silaha za nyuklia. Ni marufuku pia kwa mataifa kuhifadhia taifa jingine silaha za nyuklia katika himaya yake, au kusaidia au kuhimiza wengine kuhusika na mambo yaliyokatazwa na mkataba huu.

Mfumo wa kumaliza silaha za nyuklia

Mkataba umeweka mfumo wa kisheria uwezao kuthibitishwa na uliobadilika wa kumaliza miradi ya silaha za nyuklia na vifaa au nyenzo husika. Taifa lenye silaha za nyuklia ambalo linajiunga na mkataba halina budi kuondoa silaha zake za nyuklia zisitumike kamwe na ziharibiwe kuambatana na mpango uliokubaliwa, chini ya muda uliowekwa na ndani ya muda wa miaka 10. Taifa pia linaweza kwanza kuharibu silaha zake za nyuklia kabla ya kujiunga na mkataba na kuhakikisha hatua hiyo inathibitishwa na mamlaka teule ya kimataifa.

Kuwasaidia waathiriwa na urekebishaji wa mazingira

Mkataba unayataka mataifa kuwasaidia waathiriwa wa utumiaji na majaribio ya silaha za nyuklia. Misaada hiyo ni pamoja na huduma za matibabu, kuwawezesha kuishi maisha ya kawaida na misaada ya kisaikolojia. Ni lazima pia yachukue hatua za kurekebisha maeneo yaliyochafuliwa kwa nururishi kutoka kwa milipuko ya nyuklia. Utekelezwaji wa kufaa na utakaoleta matokeo yanayotarajiwa wa kanuni hizi utategemea ushirikiano wa kimataifa.

Kutegemea na kujenga juu ya msingi wa mikataba mingine

Mkataba wa TPNW unatilia mkazo mikataba ya awali kuhusiana na silaha za nyuklia, ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Kuzuia Ueneaji wa Silaha za Nyuklia wa 1968, ambao ulilenga kupunguza idadi ya mataifa yenye silaha za nyuklia na kuendeleza shabaha ya upunguzaji wa silaha hizo.

Kama ilivyothibitishwa na Mahakama ya Kimataifa mnamo 1996, mataifa yana jukumu la kisheria “kufuatilia kwa nia njema na kuhitimisha mashauriano kwa lengo la kupunguza silaha za nyuklia”. Kukwama kwa jukumu hili kulishawishi pakubwa mashauriano ya TPNW.

Mikataba mingine ya kukamilishana ni pamoja na Mkataba wa Kupiga Marufuku Majaribio ya Silaha za Nyuklia wa 1996 na mikataba ya kanda ya kutenga maeneo yasiyo na silaha za nyuklia katika Amerika Kusini na Caribbean, Kusini mwa Pacific, Afrika, kusini mashariki mwa Esia na Esia ya Kati.

Msingi wa TPNW ni Sheria ya Kimataifa ya Ubinadamu, ambayo imeweka mipaka ya mbinu na jinsi ya kuendeleza vita. Ni lazima makundi yanayopigana yajizuie kutumia silaha zisoweza kubagua kati ya raia na wapiganaji, ama silaha zinazosababisha majeraha yaliyopita kiasi ama mateso yasiyofaa.

Nakala ya asili ya mkataba wa TPNW. Picha na: ICAN

Kushirikisha mataifa zaidi katika TPNW

Taifa lolote linaweza kujiunga na TPNW wakati wowote. Nchi ambazo kwa sasa zinajikokota huenda zikabadili msimamo wake kwani idadi ya wanachama inazidi kuongezeka, nayo matakwa ya raia wao yanazidi kuelezwa kwa sauti ya juu zaidi.

Hali imekuwa ni hiyo hiyo kwa mikataba mingine ya awali. Kwa mfano, Ufaransa na Uchina zilipinga Mkataba wa Kuzuia Ueneaji wa Silaha za Nyuklia ulipoanza kutekelezwa lakini zikalazimika kuuridhia miongo kadhaa baadaye.

Ulimwengu unabadilika kasi na viongozi wa sasa hawatabaki mamlakani daima. Huenda serikali zijazo zikakubali manufaa ya mkataba huo ambao serikali za sasa zinakataa.

Mataifa ambayo yameridhia TPNW yanahitaji kuhimiza wengine kuungana nao kwa lengo la kufikia ufuasi wa wote duniani.

Kwa kuridhia mkataba huo, mataifa yanawasilisha ujumbe wa wazi kwamba silaha za nyuklia haziwezi kukubalika na ni lazima zikomeshwe. Wakati huu ambapo pana ongezeko la hatari za silaha za nyuklia, mkataba wa TPNW unatoa matumaini makubwa ya kumaliza silaha hizo mbaya zaidi.

“Tunafaa sasa kutwaa nafasi za kipekee zilizoletwa na mkataba huu na kukomesha enzi ya silaha za nyuklia.”

Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu, 2020

Mkutano wa mataifa yaliyotia sahihi mkataba wa TPNW uliofanyika New York mnamo 2025. Picha na: ICAN

Waliopunguza silaha: Afrika Kusini na Kazakhstan

Watetezi wawili wakuu wa TPNW, Afrika Kusini na Kazakhstan, wamethibitisha kwa vitendo vyao vya awali kuwa inawezekana kupunguza silaha za nyuklia.

Kazakhstan ilipojinyakulia uhuru mnamo 1991 kufuatia kuvunjika kwa Jamhuri ya Muungano wa Kisoshalisti ya Urusi, silaha za nyuklia zaidi ya 1,400 zilibaki ndani ya mipaka yake. Iliamua kuziondoa zote, ikitambua kwamba njia bora ya kuupata usalama wake ilikuwa ni kuondoa silaha hizo zote.

Afrika Kusini ilifikia uamuzi sawa baada ya enzi ya ubaguzi wa rangi kufika kikomo mapema miaka ya 1990. Kwa hiari yake, nchi hiyo ilibomoa maghala yote ya mabomu ya nyuklia – kitendo kilichothibitishwa baadaye na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA).

Viongozi wa mataifa hayo mawili wametangaza kuwa wanajivunia pakubwa mchango wao katika kuhakikisha ulimwengu unamaliza silaha zote za nyuklia. Wanawahimiza wengine kuwaiga.

Makasha ya mabomu ya nyuklia ya Afrika Kusini.

Hatua zifaazo kuchukuliwa kumaliza silaha za nyuklia

Binadamu ndio waliojenga silaha za nyuklia kwa mikono yao na ni wao pekee wanaoweza kuzibomoa kwa mikono hiyo hiyo. Hapana pingamizi zozote za kiufundi, na zilizopo ni za kisiasa pekee. Makumi ya maelfu ya silaha za nyuklia yamebomolewa.

Maendeleo zaidi katika kupunguza na hatimaye kumaliza silaha za nyuklia yanaweza kupatikana pakiwa na uongozi ulio tayari kuleta matokeo yanayotarajiwa na nia njema ya kisiasa. Ukweli kwamba maeneo makubwa ya ulimwengu yametangazwa kuwa hayana silaha zozote za nyuklia ni kidokezo huenda ulimwengu wote ukawa huru kutokana na silaha hizo.

Baadhi ya mielekeo mipya katika ushindani wa kihistoria wa kumiliki na kusimamia silaha za nyuklia ilipatikana wakati wa upeo wa migogoro ya kimataifa. Hali ya wasiwasi mkubwa inaweza kushawishi fikra za viongozi na kuwalazimisha kutafuta njia mpya za kuendelea mbele.

Lakini mafanikio hutegemea iwapo pana ufuasi mkubwa mashinani unaotetea mabadiliko na kushirikisha raia wahusika wa tabaka zote. Mwiko wa kimataifa ulio thabiti na wa kudumu dhidi ya silaha za nyuklia unatokana na juhudi za miongo mingi za kupinga silaha hizo.

Watu binafsi wanazo njia nyingi za kutumia kuchangia harakati za kumaliza silaha mbaya zaidi duniani. Zifuatazo ni baadhi yake:

Waandamaji waliobeba mienge wapitia jijini Oslo, Norway, wakiunga mkono TPNW. Picha na: Kristian Laemmle-Ruff

Elimisha

Wapashe habari marafiki, jamaa na wenzako mfanyao kazi pamoja kuhusu haja ya dharura ya kumaliza silaha za nyuklia. Andika makala na barua kwa wahariri, chapisha makala na picha katika mitandao ya jamii, andaa mikutano ya hadhara, vikao vya mafunzo na kuonyesha filamu.

Ni muhimu kabisa kuelimisha watu kuhusu madhara ya silaha za nyuklia kwa binadamu na mazingira. Mara nyingi, mafundisho kuhusu silaha za nyuklia huangazia tu watu waliounda na kuangusha mabomu ya nuklia mnamo 1945.

Ushahidi wa moja kwa moja wa manusura wa Hiroshima na Nagasaki, na mahojiano na walioathiriwa katika majaribio ya silaha za nyuklia, zinaweza kusaidia kubadilisha misimamo na kuhimiza kuchukuliwa kwa hatua zifaazo.

Korongo za karatasi

Nchini Japan, korongo za karatasi ni ishara ya kitamaduni ya afya njema na maisha marefu. Hata leo, korongo hizo za karatasi zinatambuliwa kimataifa kuwa ishara ya amani, na inaweza kutumiwa kuchochea mjadala muhimu kuhusu haja ya dharura ya kumaliza silaha za nyuklia.

Msichana Sadako Sasaki akiwa na umri wa miaka miwili, alikumbana na mnururisho kutoka kwa bomu la Hiroshima. Miaka kadhaa baadaye, aligunduliwa kuwa na kansa ya damu (lukemia) – ugonjwa ambao unatokana na athari zilizokawia za mnururisho – na akajiwekea shabaha ya kutengeneza korongo 1,000 za karatasi akiwa hospitalini, kwa matumaini kwamba jambo hilo lingemrejeshea afya nzuri.

Alivumilia na akatimiza lengo lake lakini kwa bahati mbaya, hali yake iliendelea kuzorota siku baada nyingine na akaaga dunia akiwa na umri wa miaka 12.

Tangu wakati huo, watoto kote Japan wamekuwa wakitengeneza korongo za karatasi ikiwa ni ishara yao ya kuunga mkono juhudi za kumalizwa kwa silaha za nyuklia.

Ni kwa nini basi msiwatumie barua au kuwapelekea korongo hao wa karatasi wajumbe wa kuchaguliwa katika nchi zenu, pamoja na barua kuwaomba kuunga mkono Mkataba wa Kupiga Marufuku Silaha za Nyuklia?

Maelfu ya korongo za karatasi zilizoupamba mnara wa ukumbusho katika Nagasaki. Credit: ICAN

Tetea

Waandikie, wapigie simu au ukutane na wenye mamlaka ya kutoa maamuzi katika nchi yako ili kujaribu kuwaomba kuunga mkono juhudi za kumaliza kabisa silaha za nyuklia.

Tangu 2017, maelfu ya wabunge kote ulimwenguni wanaowakilisha milengo tofauti ya kisiasa wameitikia masikitiko ya raia wao na kutia sahihi kiapo cha shirika la Kampeni ya Kimataifa ya Kukomesha Silaha za Nyuklia (ICAN) kuwataka watetee kuzingatiwa kwa Mkataba wa Kupiga Marufuku Silaha za Nyuklia.

Mamia ya miji mikuu, kutoka Washington DC hadi Paris hadi Sydney, inaunga rasmi mkataba huo na kutia sahihi ombi la ICAN.

Ili sauti yako isikike, si lazima uwe mtaalamu. La muhimu ni kwamba unatambua uzito wa tisho linalotukabili na umuhimu wa kuchukua hatua za haraka.

ICAN yawaleta pamoja wabunge kutoka kote ulimwenguni. Picha na: Derek French

Pinga

Maandamano ya amani ni njia muhimu ya watu kueleza uamuzi wao kukataa silaha za nyuklia. Kuna njia nyingi za kuandamana, ikiwa ni pamoja na mikutano ya hadhara, kuzingira afisi muhimu, kuandamana barabarani na shughuli za mkesha.

Kwa miongo mingi, watetezi wa amani duniani na upunguzaji wa silaha hatari, wamekuwa wakifanya maandamano, makubwa na madogo, kwa lengo la kuhakikisha ujumbe wao unawafikia wafaao. Wamekusanyika kwa mara zisizohesabika katika maeneo ya kuundia silaha za nyuklia, katika vyuo vikuu vinavyohusika na ustawishaji wa silaha hizo, na nje ya majengo ya bunge za kitaifa.

Maandamano hayo, bila shaka, yamesaidia kukomeshwa kwa majaribio ya silaha za nyuklia, kusimamishwa kwa upanuzi wa maghala na kuongezwa kwa silaha za nyuklia, kuzuia utumiaji wowote wa silaha za nyuklia tangu 1945 na kushinikiza mataifa kupunguza silaha hizo.

Hatua zaidi za moja kwa moja zinahitajika leo.

Shughuli ya kupinga silaha za nyuklia jijini Melbourne, Australia. Picha na: Jesse Boylan

Komesha uwekezaji

Katika baadhi ya mataifa yenye silaha za nyuklia, kampuni zinahusika katika uundaji wa silaha hizo na pia kutengeneza sehemu zinazohitajika za zana hizo. Mashirika ya kifedha nayo hutoa pesa zinazowezesha shughuli hizo kuendelezwa.

Kuacha kuwekeza kwa shughuli za silaha za nyuklia ni mchango unaoonekana ambao mashirika ya kifedha yanaweza kuzingatia ili kufanikisha kupunguzwa kwa silaha hizo. Mamia yamefanya hivyo na kujitolea kuhakikisha yatagharamia tu shughuli zisizo za kutengeneza silaha za nyuklia kufungamana na Mktaba wa Kupiga Marufuku Silaha za Nyuklia.

Watu binafsi wanaweza kuwasiliana na benki zao na hazina za malipo ya uzeeni na kusisitiza kwamba mashirika hayo yasiwekeze kwa kampuni zinazohusika na silaha za nyuklia.

Kuhusu ICAN

Shirika la Kampeni ya Kimataifa ya Kukomesha Silaha za Nyuklia (ICAN) ni muungano wa kimataifa wa mashirika yasiyo ya serikali wenye lengo moja kuu: kushawishi kila taifa duniani kuridhia na kutekeleza kikamilifu mkataba wa kihistoria wa kupiga marufuku silaha za nyuklia.

ICAN ilianzishwa Melbourne, Australia, mnamo 2007. Waanzilishi wake walitiwa moyo na kampeni iliyofanikiwa ya kupiga marufuku mabomu ya kutegwa ardhini mnamo 1997 kutokana na sababu za kibinadamu. Makao makuu ya ICAN leo yapo Geneva, Uswisi.

“Tunahitaji watu duniani wakate shauri kupigania kupigwa marufuku kwa silaha za nyuklia. Ili kizazi cha sasa kifikie lengo hilo, tunahitaji kujenga wimbi la maoni ya umma litakalotoa sauti kubwa kabisa: halaiki kubwa, yenye mfuro wa mawimbi, isiyozuilika na itakayotubeba hadi kuhakikisha silaha za nyuklia zimemalizwa kabisa. Bila hilo, hata viongozi wenye kipawa cha kuleta mzinduko kiasi gani watasita njiani.”

– Bill Williams, mwanzilishi mwenza wa ICAN, 2006

Shughuli ya ICAN katika Geneva. Picha na: Aude Catimel

Tangu lilipoanzishwa, ICAN limelenga kujenga wimbi nzito la umma kupinga silaha za nyuklia, ikiwa ni pamoja na kupaaza sauti za manusura wa mabomu ya nyuklia ya Hiroshima na Nagasaki, na waathiriwa wa majaribio ya silaha za nyuklia.

Ikishirikiana na Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu, makao makuu ya Umoja wa Mataifa na serikali zinazounga mkono kampeni yake, ICAN imeandaa shughuli za uhamasishaji, ikachapisha utafiti tangulizi, ikaandaa siku za kimataifa kuhimiza watu kuchukua hatua na kuwasilisha maombi ya moja kwa moja kwa wenye mamlaka makubwa kuwashinikiza kuchukua hatua za kumaliza silaha za nyuklia.

Ukweli: Kwa sasa, ICAN inashirikiana na mashirika [FACT]fact-partners[/FACT] katika mataifa [FACT]fact-partner-countries[/FACT].

Tuzo la Amani la Nobel

ICAN ilipata Tuzo la Amani la Nobel mnamo 2017, “kwa juhudi zake kuangazia athari za maangamizi kwa binadamu ya utumiaji wowote wa silaha za nyuklia, na kwa juhudi zake za kiuvumbuzi na za manufaa zilizofanikisha kupatikana kwa mkataba wa kupiga marufuku silaha kama hizo”.

“Ni imani yetu thabiti kwamba ICAN, imejitahidi kuliko mtu mwingine yeyote katika mwaka mmoja uliopita kuzipatia juhudi za kuupata ulimwengu usio na silaha zozote za nyuklia mwelekeo na nguvu mpya.”

– Kamati ya Nobel ya Norway, 2017

Tuzo hilo ni tendo la kushukuru na kutukuza juhudi za watetezi wasiohesabika na raia waliojali kote duniani ambao hawakuchoka, na tangu mwanzo wa enzi ya nyuklia, wametoa sauti kulalamika kuhusu silaha za nyuklia, wakisisitiza zimalizwe daima.

Hii si ndoto ya mbali, ila ni haja ya dharura. Ni lazima vizazi vijavyo viishi bila silaha hizo mbaya zaidi.

Shughuli iliyowahusisha wanafunzi katika Hiroshima. Picha na: Takeo Nakaoku

Setsuko Thurlow

Msichana Setsuko Thurlow aliyekuwa na umri wa miaka 13, alibwagwa chini na kupoteza fahamu kwenye mlipuko wa bomu la nyuklia lililoangushwa Hiroshima. Alikwama ndani ya kifusi cha jumba lililobomoka lakini hatimaye akafanikiwa kutambaa na kutoka nje.

“Wanafunzi wenzangu wengi waliokuwa ndani ya jengo hilo walichomeka wakiwa hai hadi kufa,” akakumbuka. “Nilijionea uharibifu usiowazika ulionizunguka … Harufu mbaya ya binadamu wakichomeka ilitanda kote hewani.”

Setsuko ambaye alishuhudia vielelezo vya kutisha vya vita vya nyuklia, alishirikiana na ICAN kupokea Tuzo la Nobel la 2017. “Kila sekunde ya kila siku, silaha za nyuklia zinahatarisha kila mtu tunayempenda na vyote tunavyovithamini,” akaonya Setsuko.

“Hatufai kamwe kuvumilia tena wazimu kama huu.”

Alihimiza viongozi wa dunia kutia sahihi Mkataba wa Kupiga Marufuku Silaha za Nyuklia ambao uliidhinishwa 2021. “Huu na uwe mwanzo wa mwisho wa silaha za nyuklia,” akasema.

“Jiungeni na huu mkataba; tumalize daima tisho la maangamizi ya nyuklia.”

Setsuko Thurlow kwenye sherehe ya Tuzo la Nobel la Amani nchini Norway mnamo 2017. Picha na: Jo Straube

Jiandikishe uwe ukipata risala za ICAN

Rudi juu