Hatari inayozidi kuongezeka ya kutumia silaha za nyuklia
Bado pana hatari kubwa ya kutumia silaha za nyuklia hata leo, iwe ni kimakosa au makusudi. Inaonekana kana kwamba hatari hiyo inazidi kuongezeka.
Hali hiyo inatokana na vitisho vinavyokabili mazingira ya usalama wa kimataifa, kuongezeka kwa mivutano miongoni mwa mataifa yenye silaha za nyuklia, mataifa hayo kuendelea kuongeza silaha zao za nyuklia, na kuzorota kwa kanuni na asasi za kimataifa.
Tishio hilo linazidishwa na harakati za kuimarisha uchokozi kupitia kwa saiba, teknolojia zinazopatia watumiaji uwezo wa kujitawala, na utumiaji wa akili mnemba (AI) katika shughuli za majeshi.
Kuweka silaha za nyuklia katika hali ya juu ya tahadhari – tayari kutumiwa ndani ya dakika chache baada ya kuonywa kuhusu uwezekano wa shambulio kutokea – ni mazoea hatari zaidi. Mara tu kombora la nyuklia likirushwa hewani, haliweza kurudishwa. Ni lazima lisafiri hadi kufikia lengo lake, hata kama lilirushwa kufuatia habari zisizo za kweli.
Viongozi wanapogubikwa na ukungu wa vita, wanaweza kuchukua hatua zisizotabirika wala bila sababu. Uwezekano wa kutoelewana huwa kubwa, hasa katika hali ya dhiki na vurugu.
Ndiposa inakuwa ni rahisi kubashiri jinsi kipindi cha hofu kubwa ya ghafla au cha kukosa huruma, kitendo cha kuudhi nafsi au kupokea habari za kupotosha zinaweza kuletea ulimwengu maangamizi, kwani uwezo wa kusababisha madhara na maafa makubwa ulimwenguni umo mikononi mwa watu wachache.
Kwa mara nyingi wakati wa vita ya maneno na propaganda kati ya mataifa ya Magharibi na Mashariki, ulimwengu ulikaribia sana kujipata vitani kamili ya nyuklia. Upeo wenye sifa mbaya ulitokea 1962 wakati wa mgogoro wa makombora ya Cuba uliohusu Marekani na Urusi.
Ingawa ni kweli kwamba silaha za nyuklia hazijawahi kutumika vitani tangu 1945, hali hiyo imetokana na bahati tu wala sio usimamizi mwema. Na huenda karibuni, tusiwe tena na bahati hiyo iwapo hatua thabiti hazitachukuliwa kumaliza tisho hilo.