SHARE

Athari za milipuko

Machafuko na vurumai zilizofuatia milipuko hiyo ni pamoja na wazazi waliokuwa tayari kufanya lolote wakiwatafuta watoto wao, nao watoto wakitafuta wazazi. Baadhi yao walipata tu mabaki ya mali binafsi ya wapendwa wao; wengine hawakupata chochote.

Juhudi za kukutanisha tena familia zilitatizwa na ukweli kwamba wengi walipatwa na majeraha mengi ya kuchomeka kiasi kwamba hawangetambulika kwa urahisi.

“Baada ya muda, nilichungulia nje ya makao ya kujisalimisha kutokana na mashambulizi ya mabomu kutoka angani. Niliona watu wametawanyika kote uwanjani. Uwanja karibu wote ulikuwa umefunikwa na watu. Wengi walionekana kama wamekufa kwani walitulia tuli. Hata hivyo, kulikuwa na waliokuwa wakitupatupa miguu ama kuinua mikono hapa na kule.”

– Fujio Tsujimoto, umri wa miaka mitano, Nagasaki

Baadhi ya manusura hawakuwa na majeraha yaliyoonekana lakini waliugua ghafla na kuaga dunia. Vifo vyao viliwashangaza waliofika kwanza kuwasaidia ambao hawakuwa na habari kwamba silaha mpya yenye madhara ya mnururisho ilitumika.

Wanawake wengi wajawazito katika miji hiyo walitunguliwa mimba ama wakazaa watoto waliokufa wakiwa wachanga, kwani mnururisho wa mabomu ulikuwa umeingia katika mimba. Kasoro za kuzaliwa, ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa kichwa kidogo, zikawa ni kawaida miongoni mwa watoto walioathiriwa na mabomu wakiwa ndani ya mimba za mama zao.

Nagasaki ilivyokuwa mwezi mmoja baada ya kushambuliwa. Picha na: Serikali ya Marekani

Mvulana huyu wa Nagasaki apokea msaada wa chakula baada ya jiji hilo kushambuliwa. Picha na: Yosuke Yamahata