Hiroshima na Nagasaki
Watu zaidi ya robo milioni waliuawa wakati Marekani ilipoangusha bomu mbili za nyuklia mijini miwili ya Japan ya Hiroshima na Nagasaki mnamo Agosti 1945, ikiwa ni mara ya kwanza na ya pekee kwa silaha za nyuklia kutumika vitani.
Watu wengi walichomeka na kugeuka majivu papo hapo. Wengine walikufa baada ya kuteseka kwa maumivu makubwa baada ya saa, siku au wiki kadhaa kufuatia mashambulizi hayo kwa kuchomeka, majeraha ya milipuko na magonjwa yaletwayo na mnururisho mkali. Wengine wasiohesabika walikufa baada ya miaka kwa kansa zinazosababishwa na mnururisho mkali, na magonjwa mengine.
Ili kuzuia kutokea tena kwa maovu kama hayo ya kikatili, ni lazima mataifa yachukue hatua za dharura za kumaliza silaha za nyuklia.
Katika Hiroshima na Nagasaki, uharibifu usio na kifani ulitokea na maafa makubwa yalifuatia na kuifanya hali ionekane kama kwamba siku ya kiyama ilikuwa imewadia: viwanja vya shule vilifunikwa na maiti za watoto, na miili ya wengine waliokaribia kufa. Akina mama walikuwa bado wameshika maiti za watoto wao wachanga. Matumbo ya watu wengine na vipande vya nyama za miili yao zilining’inia nje.
Wengi walikufa bila huduma zozote za kuwapunguzia maumivu na mateso waliyoyapata kwani ni hospitali chache zilizobaki, dawa na vifaa vingine vya matibabu ziliharibiwa, na madaktari wengi na wauguzi waliuawa ama kujeruhiwa. Waliofika katika miji hiyo kutoa misaada baada ya milipuko walikuwa wanahatarisha maisha yao kwa sababu ya masalio ya mnururisho.
Idadi kubwa ya waathiriwa – zaidi ya asilimia 90 – walikuwa ni raia, wakiwemo watoto takribani 38,000. Shambulizi la Hiroshima likitokea, wanafunzi karibu 8,400 wa shule ya upili ya daraja la chini walikuwa nje ya madarasa wakiunda fataki kama hatua ya raia kujikinga; 6,300 kati yao waliuawa.

