Walioponea
Wale ambao, kwa bahati nzuri, walioponea kufuatia mashambulizi ya mabomu ya nyuklia katika Hiroshima na Nagasaki, walipewa jina la Kijapani hibakusha, au “watu walioathiriwa na mlipuko”.
Wengi walivumilia maumivu na usumbufu maishani yao yote kutokana na majeraha ya mwili na akili. Baadhi yao waliachwa na makovu makubwa mwilini na kwenye nyuso zao au kuishi kwa miongo wakiwa na vigae vya vioo ndani ya miili yao.
Wanawake walikabiliwa na ugumu wa kipekee na makovu ya fedheha kwa kuhofia kurithisha watoto wao na wajukuu hitilafu za kizazi zilizosababishwa na mabomu hayo.
Ndani ya miaka michache baada ya mashambulizi hayo, walionusurika walianza kuugua magonjwa ya kansa na maradhi mengine kwa kasi ya juu ambayo haikuwa ya kawaida kutokana na athari za baadaye za mnururisho. Mnamo miaka ya mwanzo, visa vya kansa ya damu (lukemia) vilikuwa kawaida.
Ili kuutahadharisha ulimwenghu kuhusu hatari za silaha za nyuklia, manusura wengi wameeleza kuhusu yaliyowakumba 1945. Baadhi yao waliokuwa watoto wakati wa mashambulizi hayo wangali hai hata sasa na wameendeleza kazi ya kuueleza ukweli kuhusu madhara ya zana hizo.
Ujumbe huo umekuwa wazi na wa kutegemewa kwa miongo mingi: Binadamu na silaha za nyuklia hawawezi kuishi pamoja kwa amani.
Mnamo 2024, Nihon Hidankyo – muungano wa mashirika ya Japan yanayowakilisha manusura – lilishinda Tuzo la Amani la Nobel “kwa juhudi zake kujenga ulimwengu usio na silaha zozote za nyuklia na kwa kubainisha wazi kupitia kwa ushahidi wa manusura kuwa silaha za nyuklia hazifai kutumika tena kamwe”.
Utetezi wa kijasiri na thabiti wa manusura umewahamasisha watu wengi ulimwenguni kujiunga na wimbi la kutetea kumalizwa kwa zana za nyuklia.