Ubaguzi wa jamii za asili katika majaribio ya silaha za nyuklia
Imani zinazoegemea ubaguzi kulingana na asili za watu zimeendelea kuzingatiwa katika kufikia maamuzi ya kufanya majaribio ya silaha za nyuklia, huku serikali na waliokatalia mawazo ya nguvu za kikoloni wakiendelea kuamini kuwa watu wa asili wanaweza kutolewa mhanga, na ardhi zao takatifu hazina thamani na ni za mbali.
“Ardhi yetu, bahari yetu, jamii zetu na miili yetu zinabeba ‘urithi’ wa majaribio hayo hatari sasa na kwa vizazi vijavyo visivyojulikana,” Karina Lester, mwanamke wa jamii ya Yankunytjatjara Anangu kutoka Australia, kwa niaba ya makundi ya jamii asili, akatoa ushahidi katika kikao cha Umoja wa Mataifa mnamo 2017.
Kwenye harakati za kutafuta “silaha hatari zaidi zenye uwezo wa kusababisha uharibifu mkubwa na maafa mengi” wenye mamlaka wameendelea kuwatendea watu wa jamii za asili sawa ‘nungubandia’ kwa kuwatumia kwa majaribio, akasema. Ni nadra sana kwao kuombwa kibali, sembuse kutakiwa kutoa idhini, na walipewa kiasi kidogo au kunyimwa kinga kabisa.
Urithi wa sumu wa majaribio ya silaha za nyuklia umepokonya jamii nyingi uhusiano na maisha yao ya kitamaduni, hawawezi kurudi katika maeneo yao takatifu ya mababu zao ama kujipatia riziki kutoka kwa ardhi zao, mito na bahari, kama ambavyo wamekuwa wakifanya kwa karne nyingi.