SHARE

Visiwa vya Marshall: Vinavyotawaliwa na nururishi

Nerje Joseph alikuwa na umri wa miaka saba mnamo 1954 wakati Marekani ilipofanya jaribio lake kubwa zaidi la kulipua bomu ya nyuklia katika zoezi chapa, “Castle Bravo”, umbali wa kilomita 160 kutoka nyumbani kwake, Rongelap Atoll, ndani ya Visiwa vya Marshall.

Mlipuko huo ulikuwa mkubwa kuliko ilivyotarajiwa na ulisababisha kuenea kwa sumu zaidi. Anga ilibadilika kuwa rangi ya chungwa kisha waridi. Hakuna yeyote miongoni mwa wenyeji wa kisiwa hicho cha matumbawe aliyefahamu kilichofanyika.

Saa kadhaa baadaye, majivu nururishi na vipande vya matumbawe zikaanza kunyeshea nyumba zao, zikachafua ngozi zao, maji na chakula. Muda mfupi baadaye wakaanza kupata ishara za magonjwa yaletwayo na mnururisho uliopita kiasi.

Nywele zote za Nerje ziling’oka, na sawa na karibu kila mtu kisiwani, akapata majeraha ya kuchomeka mwilini.

Siku kadhaa baadaye, wenye mamlaka kutoka Marekani waliwahamisha wakazi wa Rongelap na kuwapeleka kisiwani kingine cha matumbawe kwa sababu ya hatari kubwa kwa afya zao kutokana na cheche za mnururisho kufuatia mlipuko wa bomu la nyuklia. Lakini miaka mitatu baada ya kuhamishwa, wakuu hao wa Marekani waliwahimiza kurudi Rongelap, kwani walitaka kuchunguza madhara ya afya ambayo yangesababishwa na mabaki ya mnururisho.

“Data ya aina hiyo haijawahi kupatikana,” akasema afisa mmoja wa Marekani wakati huo. “Ingawa watu hawa hawaishi kama watu wastaarabu wa nchi za magharibi, ni kweli kwamba wanakaribia sana kufanana nasi ukiwalinganisha na panya.”

Uamuzi wa kuwarudisha Rongelap wanakisiwa hao uliwaletea balaa. Walikumbana na ongezeko la aina tofauti za kansa, mimba kuharibika, watoto kuzaliwa wakiwa wafu na wengine wakiwa na dosari za kimaumbile.

Kutokana na mkusanyiko wa chembe za mnururisho zenye uzito tofauti na chembe nyingine, ikawa ni lazima Nerje afanyiwe upasuaji kuondoa kikoromeo chake. Alitamani warejelee siku za zamani za furaha kabla majaribio ya silaha za nyuklia hayajafanyika.

Kati ya 1946 na 1958, Marekani ilikuwa imefanya majaribio 67 ya kulipua mabomu ya nyuklia katika Visiwa vya Marshall. Jaribio la Castle Bravo pekee lilisababisha mlipuko uliokuwa na uzito mara 1,000 ukilinganishwa na wa bomu la Hiroshima.

Mpaka wa leo, visiwa vingi vya matumbawe si salama kwa binadamu kuishi, wala kuendesha kilimo au uvuvi.

Nerje Joseph aonyesha upara aliopata baada ya nywele kung’oka, na majeraha ya kuchomeka miguu kutokana na nururishi. Picha na: Serikali ya Marekani