Australia: Kupokonywa na bomu uwezo wa kuona
Mnamo 1953, wakati Yami Lester akiwa na umri wa miaka 10, Uingereza ilianza kufanya majaribio ya silaha za nyuklia katika Emu Field karibu na nyumbani kwao, sehemu ya mbali na miji ya Australia.
Anaikumbuka takataka ya nururishi, au ‘ukungu mweusi’ ikiifunika anga. Ukungu huo uIiwasha macho yake na miaka minne baadaye, alikuwa amepoteza kabisa uwezo wa kuona.
“Nilikuwa tu nacheza na watoto wengine. Ni wakati huo ambapo bomu lililipuka.” Akavuta kumbukizi. “Ninaikumbuka sauti iliyotokea, ilikuwa sauti isiyo ya kawaida, haikuwa ya juu, sio kama sauti ambayo nimewahi kusikia awali. Wakati huo huo ardhi ilitetemeshwa na tungehisi sehemu yote ikisonga.”
Saa kadhaa baadaye, kila mtu katika jamii yake alianza kuugua. “Sote tulikuwa tunatapika; tukaharisha, ngozi zikatuwasha, na macho yakauma,” akasema. “Baadhi ya wazee miongoni mwetu walikufa.”
Hatimaye, Yami akawa mtetezi wa watu asili ya Australia walioathiriwa na majaribio hayo. Hata baada ya kifo chake 2017, watoto wake wameendeleza juhudi zake kutetea haki.
