Manusura na mtetezi
Mvulana wa umri wa miaka 16 kwa jina, Sumiteru Taniguchi aliponea shambulizi la bomu ya nyuklia la Nagasaki. “Mara tu nuru ya ghafula ya mlipuko ilipotokea, nilibanduliwa kutoka nyuma ya baiskeli yangu na kubwagwa chini ardhini,” akasimulia. Aliponyanyua kichwa chake, aliona watoto wote waliokuwa wakicheza karibu naye wakiwa maiti.
Ingawa alikuwa umbali wa karibu kilomita mbili kutoka kwenye kitovu cha mlipuko, alipata majeraha mabaya ya kuchomeka mgongoni, mkono wa kushoto na mguu. Muda mfupi baadaye, majeraha hayo yaliambukizwa vidudu na kuenea, na ikabidi akae hospitalini kwa karibu miaka minne akitibiwa, ikiwa ni pamoja na miezi 21 aliyolazimika kulala kifudifudi.
Uchungu kutoka kwa majeraha hayo haukuisha. Alijitolea kwa sehemu kubwa ya maisha yake kutetea kupigwa marufuku kwa silaha za nyuklia.
